UFAFANUZI MAKATO NA TOZO UREJESHAJI MIKOPO ELIMU YA JUU
Wadau mbali mbali wa elimu nchini, wametoa maoni yao juu ya urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu, kupitia vyombo vya habari siku ya tarehe 2 february mpaka tarehe 3 february mwaka 2021, huku wakigusia zaidi juu ya makato na tozo kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu.
Kupitia maoni hayo, pamoja na mambo mengine, wadau wetu wamezungumzia viwango vya makato na tozo ambazo tumeona ni vema kutoa ufafanuzi wa viwango sahihi ili kuongeza uelewa wa wateja wetu na wananchi kwa ujumla kama ifuatavyo:
Makato ya asilimia 15 kutoka mshahara ghafi wa mnufaika si riba: Makato haya si riba kama baadhi ya wadau na vyombo vya habari vilivyoeleza. Haya ni makato pekee ya jumla anayokatwa mnufaika kutoka katika mshahara wake wa mwezi ambayo huwasilishwa HESLB na mwajiri kabla ya tarehe 15 ya mwezi unaofuata;
Baada ya kuwasilishwa HESLB, fedha hizo huingizwa katika akaunti ya mnufaika ili kupunguza deni lake, kulipa tozo mbili au tatu kulingana na deni la mnufaika – wapo wenye adhabu kwa kuchelewa kuanza kurejesha na wapo wasio na adhabu.
Aina ya tozo na umuhimu wake:
Tozo ya Uendeshaji (Asilimia 1): Hii hukatwa mara moja tu kwa mkupuo wakati mnufaika anapowasilisha makato ya kwanza. Lengo la tozo hii ni kugharamia uendeshaji wa shughuli za urejeshaji mikopo kama kuwasaka manufaika; kuandaa ankara n.k;
Tozo ya Kutunza Thamani ya Fedha za Mkopo (Asilimia 6): Tozo hii hutozwa kwa mwaka katika deni lililosalia (Outstanding Loan Balance) na sio kwenye deni la msingi (Principal Loan).
Lengo la tozo hii ni kuiwezesha Serikali, kupitia HESLB, kuwa na mfuko endelevu utakaowezesha kukopesha wahitaji wengine bila kuathiri thamani ya fedha za mkopo ambazo mnufaika alipokea akiwa masomoni.
Adhabu ya asilimia 10 kwa wanufaika wanaochelewa kurejesha: Hii ni adhabu inayolenga kuwakumbusha wanufaika umuhimu wa kuanza kurejesha mapema. Baada ya mwaka 2016, adhabu hii ilianza kutozwa miezi 24 baada ya mnufaika kuhitimu masomo. Kabla ilikua miezi 12 baada ya kuhitimu.
Tunapenda kuwakumbusha wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu ambao hawajajitokeza, kujitokeza na kuanza kurejesha ili kuepuka adhabu na kumaliza madeni yao ili wahitaji wengine wanufaike.
Comments
Post a Comment